[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13]

Chapter 7

1: Basi, wapenzi wangu, tukiwa tumepewa ahadi hizi zote, na tujitakase na chochote kiwezacho kuchafua miili na roho zetu, tuwe watakatifu kabisa, na tuishi kwa kumcha Mungu. 2: Tunaomba mtupe nafasi mioyoni mwenu! Hatujamkosea mtu yeyote, hatujamdhuru wala kumdanganya mtu yeyote. 3: Sisemi mambo haya kwa ajili ya kumhukumu mtu; maana, kama nilivyokwisha sema, ninyi mko mioyoni mwetu, tufe pamoja, tuishi pamoja. 4: Nina imani kubwa sana ninaposema nanyi; naona fahari kubwa juu yenu! Katika taabu zetu nimepata kitulizo kikubwa na kufurahi mno. 5: Hata baada ya kufika Makedonia hatukuweza kupumzika. Kila upande tulikabiliwa na taabu: nje ugomvi; ndani hofu. 6: Lakini Mungu, mwenye kuwapa shime wanyonge alitupa moyo sisi pia kwa kuja kwake Tito. 7: Si tu kwa kule kuja kwake Tito, bali pia kwa sababu ya moyo mliompa ninyi. Yeye ametuarifu jinsi mnavyotamani kuniona, jinsi mlivyo na huzuni, na mnavyotaka kunitetea. Jambo hili linanifurahisha sana. 8: Maana, hata kama kwa barua ile yangu nimewahuzunisha, sioni sababu ya kujuta. Naam, naona kwamba barua hiyo iliwatia huzuni lakini kwa muda. 9: Sasa nafurahi, si kwa sababu mmehuzunika, ila kwa kuwa huzuni yenu imewafanya mbadili nia zenu na kutubu. Mmehuzunishwa kadiri ya mpango wa Mungu, na kwa sababu hiyo hatukuwadhuru ninyi kwa vyovyote. 10: Kuwa na huzuni jinsi atakavyo Mungu, husababisha badiliko la moyo, badiliko lenye kuleta wokovu; hivyo hakuna sababu ya kujuta. Lakini huzuni ya kidunia huleta kifo. 11: Sasa mnaweza kuona matokeo ya kuona huzuni jinsi Mungu atakavyo: ninyi mmepata kuwa sasa watu wenye jitihada, wenye hoja, mnashtuka na kuogopa, mna bidii na mko tayari kuona kwamba haki yatekelezwa. Ninyi mmethibitisha kwa kila njia kwamba hamna hatia kuhusu jambo hili. 12: Hivyo, ingawa niliandika ile barua, haikuwa kwa ajili ya yule aliyekosa, au kwa ajili ya yule aliyekosewa. Niliandika kusudi ionekane wazi mbele ya Mungu jinsi mlivyo na bidii kwa ajili yetu. 13: Ndiyo maana sisi tulifarijika sana. Siyo kwamba tulifarijika tu, ila pia Tito alitufurahisha kwa furaha aliyokuwa nayo kutokana na jinsi mlivyomchangamsha moyo. 14: Mimi nimewasifu sana mbele yake, na katika jambo hilo sikudanganyika. Tumewaambieni ukweli daima, na kule kuwasifia ninyi mbele ya Tito kumekuwa jambo la ukweli mtupu. 15: Hivyo upendo wake wa moyo kwenu unaongezeka zaidi akikumbuka jinsi ninyi nyote mlivyo tayari kutii, na jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu nyingi na kutetemeka. 16: Nafurahi sana kwamba naweza kuwategemea ninyi kabisa katika kila jambo.