[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13]

Chapter 6

1: Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure. 2: Mungu asema hivi: "Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia." Basi, sasa ndio wakati wa kufaa, sasa ndiyo siku ya wokovu! 3: Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuio chochote. 4: Badala yake, tunajionyesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu. 5: Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula. 6: Tunajionyesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki, 7: kwa ujumbe wa kweli na kwa nguvu ya Mungu. Uadilifu ndiyo silaha yetu upande wa kulia na upande wa kushoto. 8: Tuko tayari kupata heshima na kudharauliwa, kulaumiwa na kusifiwa. Twadhaniwa kuwa waongo, kumbe twasema kweli; 9: kama wasiojulikana, kumbe twajulikana kwa wote, kama waliokufa, lakini mwonavyo, sisi ni wazima kabisa. 10: Ingawa tumeadhibiwa, hatukuuawa; ingawa tunayo huzuni, twafurahi daima; ingawa tu maskini hohehahe, lakini twatajirisha watu wengi; twaonekana kuwa watu tusio na chochote, kumbe tuna kila kitu. 11: Ndugu Wakorintho, tumezungumza nanyi kwa unyofu; mioyo yetu iko wazi kabisa. 12: Kama mnaona kuna kizuizi chochote kile, kizuizi hicho kiko kwenu ninyi wenyewe, na si kwa upande wetu. 13: Sasa nasema nanyi kama watoto wangu, wekeni mioyo yenu wazi kama nasi tulivyofanya. 14: Msiambatane na watu wasioamini. Je, wema na uovu vyapatana kweli? Mwanga na giza vyawezaje kukaa pamoja? 15: Kristo anawezaje kupatana na Shetani? Muumini ana uhusiano gani na asiyeamini? 16: Hekalu la Mungu lina uhusiano gani na sanamu za uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu mwenyewe alivyosema: "Nitafanya makao yangu kwao, na kuishi kati yao; Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu." 17: Kwa hiyo Bwana asema pia: "Ondokeni kati yao, mkajitenge nao, msiguse kitu najisi, nami nitawapokea. 18: Mimi nitakuwa Baba yenu, nanyi mtakuwa watoto wangu, waume kwa wake, asema Bwana Mwenye Uwezo."