[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13]

Chapter 1

1: Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, tunawaandikia ninyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho, na watu wote wa Mungu kila mahali katika Akaya. 2: Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo. 3: Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote. 4: Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu. 5: Naam, kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyohiyo tunazidi kufarijiwa naye. 6: Ikiwa tunapata taabu, basi ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu. Tukifarijika, ni kwa ajili ya kuwafariji ninyi na kuwaunga mkono mpate nguvu ya kustahimili mateso yaleyale tunayoteseka sisi. 7: Tena, matumaini tuliyo nayo kwa ajili yenu ni imara; tunajua kwamba mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu. 8: Ndugu, tunataka kuwajulisheni taabu zilizotupata kule Asia; taabu hizo zilitulemea kupita kiasi, hata tukakata matumaini yote ya kuendelea kuishi. 9: Naam, tulikuwa kama watu waliohukumiwa kuuawa, ili tufundishwe kumtegemea Mungu mwenye kuwafufua wafu, badala ya kutegemea nguvu zetu sisi wenyewe. 10: Yeye alituokoa katika hatari kubwa ya kifo, na anaendelea kutuokoa; sisi tumemwekea tumaini letu kwamba atatuokoa tena, 11: ninyi mkiwa mnatuunga mkono kwa kutuombea. Hivyo neema tutakazokuwa tumepata kutokana na maombi ya watu wengi hivyo, ziwe sababu ya watu wengi zaidi kumshukuru Mungu kwa ajili yetu. 12: Sisi tunajivunia kitu kimoja: dhamiri yetu inatuhakikishia kwamba tumeishi ulimwenguni hapa, na hasa kati yenu, kwa unyenyekevu na unyofu tuliojaliwa na Mungu; hatukuongozwa na hekima ya kibinadamu bali neema ya Mungu. 13: Tunawaandikia ninyi mambo mnayoweza kuyasoma na kuyaelewa. Ninatumaini kwamba mtaelewa vizuri kabisa, 14: maana mpaka sasa mmenielewa kiasi fulani tu. Tunajua kwamba katika ile Siku ya Bwana Yesu mtaweza kutuonea sisi fahari kama nasi tunavyowaonea ninyi fahari. 15: Nikiwa na matumaini hayo, nilikusudia kuja kwenu hapo awali ili mpate baraka maradufu. 16: Nilikusudia kupita kwenu nikiwa safarini kwenda Makedonia, na wakati wa kurudi pia, ili nipate msaada wenu kwa safari yangu kwenda Yudea. 17: Je, mnadhani nilipopanga hivyo nimekuwa kama mtu asiye na msimamo? Je, mnadhani kwamba ninafanya uamuzi wangu kwa fikira za kibinadamu na kwamba nasema "Ndiyo" na "Siyo" papo hapo? 18: Mungu ni ukweli mtupu; basi, kile tulichowaambia ninyi si jambo la "Ndiyo" na "Siyo". 19: Maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silwano na Timotheo, tulimhubiri kwenu, hakuwa mtu wa "Ndiyo" na "Siyo"; bali yeye daima ni "Ndiyo" ya Mungu. 20: Maana ndani yake ahadi zote za Mungu zimekuwa "Ndiyo". Kwa sababu hiyo, "Amina" yetu husemwa kwa njia ya Kristo kwa ajili ya kumtukuza Mungu. 21: Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na ninyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu; 22: ndiye aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea. 23: Mungu ndiye shahidi wangu--yeye anajua moyo wangu! Mimi sikuja tena Korintho, kwa sababu tu ya kuwahurumieni. 24: Hatutaki kutumia mabavu juu ya imani yenu; ninyi mko imara katika imani yenu. Wajibu wetu ni kufanya kazi pamoja kwa ajili ya furaha yenu.