[1] [2] [3] [4] [5] [6]

Chapter 4

1: Roho asema waziwazi kwamba siku za baadaye watu wengine wataitupilia mbali imani; watazitii roho danganyifu na kufuata mafundisho ya pepo. 2: Mafundisho ya namna hiyo yanaenezwa na watu waongo wadanganyifu, ambao dhamiri zao ziko kama zimechomwa kwa chuma cha moto. 3: Watu hao hufundisha kwamba ni makosa kuona na pia kula vyakula fulani. Lakini Mungu aliviumba vyakula hivyo, ili wale walio waumini na ambao wanapata kuujua ukweli, wavitumie kwa shukrani. 4: Kila kitu alichoumba Mungu ni chema, wala hakuna kinachohitaji kukataliwa, bali vyote vipokelewe kwa sala ya shukrani, 5: kwa sababu neno la Mungu na sala hukifanya kitu hicho kikubalike kwa Mungu. 6: Kama ukiwapa ndugu wote maagizo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, ukijiendeleza kiroho kwa maneno ya imani na mafundisho ya kweli, ambayo wewe umeyafuata. 7: Lakini achana na hadithi zile zisizo za kidini na ambazo hazina maana. Jizoeshe kuishi maisha ya uchaji wa Mungu. 8: Mazoezi ya mwili yana faida yake, lakini mazoezi ya kiroho yana faida za kila namna, maana yanatuahidia uzima katika maisha ya sasa, na pia hayo yanayokuja. 9: Usemi huo ni wa kusadikika kabisa na unastahili kukubaliwa. 10: Sisi tunajitahidi na kufanya kazi kwa bidii kwani tumemwekea tumaini letu Mungu aliye hai ambaye ni Mwokozi wa watu wote, na hasa wale wanaoamini. 11: Wape maagizo hayo na mafundisho hayo. 12: Usikubali mtu yeyote akudharau kwa sababu wewe ni kijana, lakini jitahidi uwe mfano kwa wanaoamini: katika usemi wako, mwenendo wako, upendo, imani na maisha safi. 13: Tumia wakati wako na juhudi yako katika kusoma hadharani Maandiko Matakatifu, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja. 14: Usiache kukitumia kile kipaji cha Kristo ndani yako ulichopewa kwa maneno ya manabii na kwa kuwekewa mikono na wazee. 15: Fikiri kwa makini juu ya hayo yote na kuyatekeleza kusudi maendeleo yako yaonekane na wote. 16: Angalia sana mambo yako mwenyewe, na mafundisho yako. Endelea kufanya hayo maana ukifanya hivyo utajiokoa mwenyewe na wale wanaokusikiliza.