[1] [2] [3] [4] [5] [6]

Chapter 2

1: Kwanza kabisa, basi naomba dua, sala, maombi na sala za shukrani zitolewe kwa Mungu kwa ajili ya watu wote, 2: kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema. 3: Jambo hili ni jema na lampendeza Mungu Mwokozi wetu, 4: ambaye anataka watu wote waokolewe na wapate kuujua ukweli. 5: Maana yuko Mungu mmoja, na pia yuko mmoja anayewapatanisha watu na Mungu, binadamu Kristo Yesu, 6: ambaye alijitoa mwenyewe kuwakomboa watu wote. Huo ulikuwa uthibitisho, wakati ufaao ulipowadia. 7: Kwa sababu hiyo mimi nilitumwa niwe mtume na mwalimu wa watu wa mataifa, niutangaze ujumbe wa imani na ukweli. Nasema ukweli; sisemi uongo! 8: Basi, popote mnapokutana kufanya ibada nataka wanaume wasali, watu waliojitolea kweli na ambao wanaweza kuinua mikono yao wakisali bila hasira wala ubishi. 9: Hali kadhalika, nawataka wanawake wawe wanyofu na wenye busara kuhusu mavazi yao; wavae sawasawa na si kwa urembo wa mitindo ya kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa, 10: bali kwa matendo mema kama iwapasavyo wanawake wamchao Mungu. 11: Wanawake wanapaswa kukaa kimya na kuwa wanyenyekevu wakati wa kujifunza. 12: Mimi simruhusu mwanamke amfundishe au amtawale mwanamume; anapaswa kukaa kimya. 13: Maana Adamu aliumbwa kwanza, halafu Hawa. 14: Na wala si Adamu aliyedanganywa; bali mwanamke ndiye aliyedanganywa, akaivunja sheria ya Mungu. 15: Hata hivyo, mwanamke ataokolewa kwa kupata watoto, kama akidumu katika imani, upendo, utakatifu na unyofu.