[1]
[2]
[3]
[4]
[5]
Chapter 51:
Ndugu, hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya nyakati na majira yatakapotukia mambo haya.
2:
Maana ninyi wenyewe mwajua kwamba Siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajavyo usiku.
3:
Watu watakapokuwa wanasema: "Kila kitu ni shwari na salama" ndipo uharibifu utakapowaangukia ghafla! Mambo hayo yatatukia ghafla kama uchungu wa uzazi unavyomjia mama anayejifungua, wala watu hawataweza kuepukana nayo.
4:
Lakini ninyi ndugu, hamko gizani, na siku hiyo haipaswi kuwajieni ghafla kama vile mwizi.
5:
Ninyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza.
6:
Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi.
7:
Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku.
8:
Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma.
9:
Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,
10:
ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au tumekufa.
11:
Kwa hiyo farijianeni na kusaidiana ninyi kwa ninyi kama mnavyofanya sasa.
12:
Ndugu, tunawaombeni muwastahi wale wanaofanya kazi kati yenu, wale wanaowaongoza na kuwafundisheni kuhusu maisha ya Kikristo.
13:
Wapeni heshima kubwa na kuwapenda kwa sababu ya kazi wanayofanya. Muwe na amani kati yenu.
14:
Ndugu, tunawahimizeni muwaonye watu walio wavivu, muwatie moyo watu wanyonge, muwasaidie watu dhaifu, muwe na subira kwa wote.
15:
Angalieni mtu yeyote asimlipe mwingine maovu kwa maovu, ila nia yenu iwe kutendeana mema daima na kuwatendea mema watu wote.
16:
Furahini daima,
17:
salini kila wakati
18:
na muwe na shukrani katika kila hali. Hayo ndiyo anayotaka Mungu kwenu katika kuungana kwenu na Kristo Yesu.
19:
Msimpinge Roho Mtakatifu;
20:
msidharau unabii.
21:
Pimeni kila kitu: zingatieni kilicho chema,
22:
na epukeni kila aina ya uovu.
23:
Mungu anayetupatia amani awafanye ninyi watakatifu kwa kila namna na kuzilinda nafsi zenu--roho, mioyo na miili yenu--mbali na hatia yoyote wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
24:
Yeye anayewaita ninyi atafanya hivyo kwani ni mwaminifu.
25:
Ndugu, tuombeeni na sisi pia.
26:
Wasalimuni ndugu wote kwa ishara ya upendo.
27:
Nawahimizeni kwa jina la Bwana muwasomee ndugu zetu wote barua hii.
28:
Tunawatakieni neema ya Bwana wetu Yesu Kristo.
|