[1] [2] [3] [4] [5]

Chapter 4

1: Hatimaye, ndugu zangu, mmejifunza kutoka kwetu namna mnavyopaswa kuishi ili kumpendeza Mungu. Na kweli mmekuwa mnaishi hivyo. Sasa tunawaombeni na kuwasihi kwa jina la Bwana Yesu mfanye vema zaidi. 2: Maana mnayajua yale maagizo tuliyowapeni kwa mamlaka ya Bwana Yesu. 3: Mungu anataka ninyi muwe watakatifu na mjiepushe kabisa na maisha ya zinaa. 4: Kila mwanamume anapaswa kujua namna ya kuishi na mkewe kwa utakatifu na heshima, 5: na si kwa tamaa mbaya kama watu wa mataifa mengine wasiomjua Mungu. 6: Basi, mtu yeyote asimkosee au kumpunja mwenzake kuhusu jambo hili. Tulikwisha waambieni hayo na kuwaonya kwamba Bwana atawaadhibu wanaofanya mambo hayo. 7: Mungu hakutuita tuishi maisha ya zinaa, bali tuishi katika utakatifu. 8: Kwa hiyo basi, anayedharau mafundisho hayo hamdharau mtu, bali amdharau Mungu mwenyewe anayewapeni Roho wake Mtakatifu. 9: Hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya kuwapenda ndugu zenu waumini. Ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu namna mnavyopaswa kupendana. 10: Na mmekuwa mkiwatendea hivyo ndugu zenu wote kila mahali katika Makedonia. Basi, ndugu tunawaombeni mfanye hata zaidi. 11: Muwe na nia ya kuishi maisha ya utulivu, kila mmoja ashughulikie mambo yake mwenyewe na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe kama tulivyowaagiza pale awali. 12: Kwa namna hiyo mtajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo, na hamtakuwa na lazima ya kuwategemea wengine kwa mahitaji yenu. 13: Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. 14: Sisi tunaamini kwamba Yesu alikufa, akafufuka; na hivyo sisi tunaamini kwamba Mungu atawaleta pamoja na Yesu wale wote waliofariki wakiwa wanamwamini. 15: Hili tunalowaambieni ni fundisho la Bwana; sisi tulio hai, ambao tutakuwa tumebaki, wakati Bwana atakapokuja, hakika hatutawatangulia wale waliokwisha fariki dunia. 16: Maana patatolewa amri, sauti ya malaika mkuu, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza. 17: Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana. 18: Basi, farijianeni kwa maneno haya.