[1] [2] [3] [4] [5]

Chapter 3

1: Oneni basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu. 2: Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo. 3: Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo, hujiweka safi kama vile Kristo alivyo safi kabisa. 4: Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana dhambi ni uvunjaji wa sheria. 5: Mnajua kwamba Kristo alikuja kuziondoa dhambi zetu, na kwamba kwake hamna dhambi yoyote. 6: Basi, kila aishiye katika muungano na Kristo hatendi dhambi; lakini kila mtu atendaye dhambi hakupata kamwe kumwona, wala kumjua Kristo. 7: Basi, watoto wangu, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote. Mtu atendaye matendo maadilifu ni mwadilifu kama vile Kristo alivyo mwadilifu kabisa. 8: Lakini atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi ametenda dhambi tangu mwanzo. Lakini Mwana wa Mungu alikuja duniani kuiharibu kazi ya Ibilisi. 9: Kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, maana anayo hali ya kimungu ndani yake; hawezi kutenda dhambi kwa sababu yeye ni mtoto wa Mungu. 10: Lakini yeyote asiyetenda mambo maadilifu, au asiyempenda ndugu yake, huyo si mtoto wa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi. 11: Na, ujumbe mliousikia tangu mwanzo ndio huu: Tunapaswa kupendana! 12: Tusiwe kama Kaini ambaye, kwa kuongozwa na yule Mwovu, alimuua ndugu yake. Na, kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa maovu, lakini yale ya ndugu yake yalikuwa mema! 13: Basi, ndugu zangu, msishangae kama ulimwengu unawachukia ninyi. 14: Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo na kuingia katika uzima kwa sababu tunawapenda ndugu zetu. Mtu asiye na upendo hubaki katika kifo. 15: Kila anayemchukia ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua kwamba muuaji yeyote yule hana uzima wa milele ndani yake. 16: Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu. 17: Basi, mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona ndugu yake ana shida, lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma, anawezaje kusema kwamba anampenda Mungu? 18: Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe upendo wa kweli na wa vitendo. 19: Hivyo ndivyo tuwezavyo kuwa na hakika kwamba sisi ni watu wa ukweli; na hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu. 20: Kwa maana, hata kama dhamiri yetu yatuhukumu, twajua kwamba Mungu ni mkuu zaidi kuliko dhamiri, na kwamba yeye ajua kila kitu. 21: Wapenzi wangu, kama dhamiri yetu haina lawama juu yetu, basi, twaweza kuwa na uthabiti mbele ya Mungu, 22: na twaweza kupokea kwake chochote tunachoomba, maana tunazitii amri zake na kufanya yale yanayompendeza. 23: Na, amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Kristo, na kupendana kama alivyotuamuru. 24: Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na Mungu na Mungu anaishi katika muungano naye. Kwa njia ya Roho ambaye Mungu ametujalia, sisi twajua kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi.