[1] [2] [3] [4] [5]

Chapter 1

1: Habari hii ya yahusu Neno la uzima lililokuwako tangu mwanzo. Sisi tumepata kulisikia na kuliona kwa macho yetu wenyewe; tulilitazama na kulishika kwa mikono yetu wenyewe. 2: Uzima huo ulipotokea sisi tuliuona na sasa tunasema habari zake na kuwaambieni juu ya uzima huo wa milele uliokuwa kwa Baba na uliodhihirishwa kwetu. 3: Tulichokiona na kukisikia ndicho tunachowatangazieni ninyi pia ili nanyi mpate kushirikiana nasi katika umoja tulio nao na Baba na Mwanae Yesu Kristo. 4: Tunawaandikia ninyi mambo haya kusudi furaha yetu ikamilike. 5: Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake. 6: Tukisema kwamba tuna umoja naye,na papo hapo twaishi gizani, tutakuwa tumesema uongo kwa maneno na matendo. 7: Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote. 8: Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe na ukweli haumo ndani yetu. 9: Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa na uovu wote. 10: Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno lake halimo ndani yetu.