[1]
[2]
[3]
[4]
[5]
[6]
[7]
[8]
[9]
[10]
[11]
[12]
[13]
[14]
[15]
[16]
Chapter 111:
Niigeni mimi kama ninavyomwiga Kristo.
2:
Nawapeni hongera kwa sababu mnanikumbuka na kwa sababu mnayashikilia yale maagizo niliyowapeni.
3:
Lakini napenda pia mjue kwamba Kristo ni kichwa cha kila mwanamume, na mwanamume ni kichwa cha mkewe, na Mungu ni kichwa cha Kristo.
4:
Basi, kila mwanamume anayesali au anayetangaza ujumbe wa Mungu huku amefunika kichwa chake, huyo anamdharau Kristo.
5:
Na mwanamke akisali au kutangaza ujumbe wa Mungu bila kufunika kichwa chake, anamdharau mumewe; anayefanya hivyo ni sawa tu na mwanamke aliyenyoa kichwa chake.
6:
Mwanamke asiyefunika kichwa chake, afadhali anyoe nywele zake. Lakini ni aibu kwa mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa; basi, afadhali afunike kichwa chake.
7:
Haifai mwanamume kufunika kichwa chake, kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na kioo cha utukufu wake Mungu; lakini mwanamke ni kioo cha utukufu wa mwanamume.
8:
Mwanamume hakutoka kwa mwanamke, ila mwanamke alitoka kwa mwanamume.
9:
Mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, ila mwanamke aliumbwa kwa ajili ya mwanamume.
10:
Ndiyo maana mwanamke hufunika kichwa chake, iwe ishara ya mamlaka yaliyo juu yake, na pia kwa sababu ya malaika.
11:
Hata hivyo, mbele ya Bwana mwanamke si kitu bila mwanamume, naye mwanamume si kitu bila mwanamke.
12:
Kama vile mwanamke alivyotokana na mwanamume, vivyo hivyo mwanamume huzaliwa na mwanamke; kila kitu hutoka kwa Mungu.
13:
Amueni wenyewe: Je, inafaa mwanamke kumwomba Mungu bila kuvaa kitu kichwani?
14:
Hata maumbile yenyewe huonyesha wazi kwamba kwa mwanamume kuwa na nywele ndefu ni aibu kwake mwenyewe;
15:
lakini kwa mwanamke kuwa na nywele ni heshima kwake; nywele zake ndefu amepewa ili zimfunike.
16:
Kama mtu anataka kuleta ubishi juu ya jambo hili, basi, na ajue kwamba sisi hatuna desturi nyingine, wala makanisa ya Mungu hayana desturi nyingine.
17:
Nikiwa bado nawapeni maagizo haya, siwezi hata kidogo kuwapa ninyi hongera kuhusu haya yafuatayo: mikutano yenu ninyi waumini yaleta hasara zaidi kuliko faida.
18:
Awali ya yote, nasikia kwamba mnapokutana pamoja hutokea mafarakano kati yenu. Nami naamini kiasi,
19:
maana ni lazima fikira tofauti ziweko miongoni mwenu, ili wale walio thabiti wapate kutambulikana.
20:
Kweli mnakutana, lakini si kwa ajili ya kula chakula cha Bwana!
21:
Maana mnapokula kila mmoja hukikalia chakula chake mwenyewe, hata hutokea kwamba baadhi yenu wana njaa, na wengine wamelewa!
22:
Je, hamwezi kula na kunywa nyumbani kwenu! Au je, mnalidharau kanisa la Mungu na kuwaaibisha hao wasio na kitu? Niwaambie nini? Niwasifu? La hasha! Si kuhusu jambo hili.
23:
Maana mimi nilipokea kwa Bwana yale maagizo niliyowaachieni: kwamba, usiku ule Bwana Yesu aliotolewa, alitwaa mkate,
24:
akamshukuru Mungu, akaumega, akasema: "Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa kunikumbuka."
25:
Vivyo hivyo, baada ya kula, akatwaa kikombe akasema: "Hiki ni kikombe cha agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu. Fanyeni hivi, kila mnapokunywa, kwa kunikumbuka."
26:
Maana kila mnapokula mkate huu na kunywa kikombe hiki, mwatangaza kifo cha Bwana, mpaka atakapokuja.
27:
Kwa hiyo, kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana.
28:
Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe kikombe hicho;
29:
maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana, anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe.
30:
Ndiyo maana wengi kati yenu ni dhaifu na wagonjwa, na wengine kadhaa wamekufa.
31:
Kama tungejichunguza wenyewe vizuri hatungeadhibiwa hivyo.
32:
Lakini tunapohukumiwa na Bwana, tunafunzwa tuwe na nidhamu, ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.
33:
Kwa hiyo, ndugu zangu, mnapokutana kula chakula cha Bwana, kila mmoja amngoje mwenzake.
34:
Na kama kuna yeyote aliye na njaa, na ale nyumbani kwake, ili kukutana kwenu kusisababishe hukumu. Lakini, kuhusu yale mambo mengine, nitawapeni maelezo nitakapokuja.
|