[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16]

Chapter 6

1: Anathubutuje mmoja wenu kumshtaki ndugu muumini mbele ya mahakama ya watu wasiomjua Mungu badala ya kumshtaki mbele ya watu wa Mungu? 2: Je, hamjui kwamba watu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Ikiwa basi, ulimwengu utahukumiwa nanyi, kwa nini hamstahili kuhukumu hata katika mambo madogo? 3: Je, hamjui kwamba, licha ya kuhukumu mambo ya kawaida ya kila siku, tutawahukumu hata malaika? 4: Mnapokuwa na mizozo juu ya mambo ya kawaida, je, mnawaita wawe mahakimu watu ambao hata hawalijali kanisa? 5: Aibu kwenu! Ndiyo kusema hakuna hata mmoja miongoni mwenu mwenye hekima kiasi cha kuweza kutatua tatizo kati ya ndugu waumini? 6: Badala yake, kweli imekuwa mtindo ndugu kumpeleka ndugu yake mahakamani, tena mbele ya mahakimu wasioamini. 7: Kwa kweli huko kushtakiana tu wenyewe kwa wenyewe kwabainisha kwamba mmeshindwa kabisa! Je, haingekuwa jambo bora zaidi kwenu kudhulumiwa! Haingekuwa bora zaidi kwenu kunyang`anywa mali yenu? 8: Lakini, badala yake, ninyi ndio mnaodhulumu na kunyang`anya; tena, hayo mnawafanyia ndugu zenu! 9: Au je, hamjui kwamba watu wabaya hawataurithi Utawala wa Mungu? Msijidanganye! Watu wanaoishi maisha ya uasherati, wanaoabudu sanamu, wazinzi, au walawiti, 10: wevi, wachoyo, walevi, wasengenyaji, wanyang`anyi, hao wote hawatashiriki Utawala wa Mungu. 11: Baadhi yenu mlikuwa hivyo; lakini sasa mmeoshwa, mkafanywa watakatifu, na kupatanishwa na Mungu kwa jina la Bwana Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu. 12: Mtu anaweza kusema: "Kwangu mimi kila kitu ni halali." Sawa; lakini si kila kitu kinafaa. Nakubali kwamba kila kitu ni halali kwangu lakini sitaki kutawaliwa na kitu chochote. 13: Unaweza kusema: "Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya chakula." Sawa; lakini Mungu ataviharibu vyote viwili. Mwili wa mtu si kwa ajili ya uzinzi bali ni kwa ajili ya kumtumikia Bwana, naye Bwana ni kwa ajili ya mwili. 14: Basi, Mungu aliyemfufua Bwana kutoka wafu atatufufua nasi pia kwa nguvu yake. 15: Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya mwili wa Kristo? Je, mnadhani naweza kuchukua sehemu ya mwili wa Kristo na kuifanya kuwa sehemu ya mwili wa kahaba? Hata kidogo! 16: Maana, kama mjuavyo, anayeungana na kahaba huwa mwili mmoja naye--kama ilivyoandikwa: "Nao wawili watakuwa mwili mmoja." 17: Lakini aliyejiunga na Bwana huwa roho moja naye. 18: Jiepusheni kabisa na uzinzi. Dhambi nyingine zote hutendwa nje ya mwili lakini mzinzi hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe. 19: Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, ambaye mlimpokea kutoka kwa Mungu? Ninyi basi, si mali yenu wenyewe. 20: Mlinunuliwa kwa bei kubwa. Kwa hiyo, itumieni miili yenu kwa ajili ya kumtukuza Mungu.