[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16]

Chapter 5

1: Ziko habari za kuaminika kwamba kuna uzinzi miongoni mwenu; tena ni uzinzi mbaya ambao haujapata kuwako hata kati ya watu wasiomjua Mungu. Nimeambiwa eti mmoja wenu anaishi na mke wa baba yake! 2: Mnawezaje kujivuna? Ingekuwa afadhali kwenu kuomboleza, na huyo aliyefanya kitu hicho aondolewe miongoni mwenu. 3: Nami, kwa upande wangu, ingawa kwa mwili niko mbali nanyi, hata hivyo kwa roho niko hapo pamoja nanyi: na hivyo, kama vile nipo hapo, nimekwisha mhukumu huyo aliyefanya jambo hilo la aibu. 4: Wakati mnapokusanyika pamoja kwa jina la Bwana Yesu, nami nikiwa pamoja nanyi kwa roho, basi, kwa uwezo wa Bwana wetu Yesu, 5: mkabidhini mtu huyo kwa Shetani ili mwili wake uharibiwe na roho yake iweze kuokolewa Siku ile ya Bwana. 6: Majivuno yenu hayafai! Je, hamjui kwamba chachu kidogo huchachusha donge lote la unga? 7: Jitakaseni, mkatupe mbali chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu kama mnavyopaswa kuwa; maana, Kristo, Pasaka yetu, amekwisha tolewa tambiko. 8: Basi, tufanye karamu hiyo si kwa chachu ile ya kale, chachu ya ubaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, mkate wa usafi na kweli. 9: Niliwaandikia katika barua yangu msishirikiane na wazinzi. 10: Ukweli ni kwamba sikuwa na maana ya watu wote duniani walio wazinzi, wachoyo, walaghai na wenye kuabudu sanamu. Maana, ili kuwaepa hao wote ingewalazimu ninyi kuihama dunia hii kabisa! 11: Nilichoandika ni hiki: msishirikiane na ndugu Mkristo aliye mzinzi, mchoyo, mwenye kuabudu sanamu, mchongezi mlevi na mlaghai. Mtu wa namna hiyo, hata kula msile naye. 12: Je, ni shauri langu kuwahukumu watu walio nje? Hao Mungu atawahukumu. Je, ninyi hampaswi kuwahukumu wale walio katika jamii yenu ninyi wenyewe? 13: Mfukuzeni mbali nanyi huyo mwovu!